4 Juni 2024 - 20:15
UN: Wapalestina milioni moja wamelazimika kukimbia Rafah

Wapalestina zaidi ya milioni moja sasa wamefungasha virago na kuukimbia mji wa Rafah kusini mwa Gaza huku utawala katili wa Israel ukiendeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya wakimbizi katika eneo hilo.

Katika tarifa yake iliyotolewa Jumatatu  kupitia mtandao wa kijamii wa X , Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema  mji wa Rafah kwenye mpaka wa kusini wa Gaza na Misri ulikuwa umewapa hifadhi zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao kwa karibu miezi minane ya mashambulizi ya kila siku ya jeshi la Israel tangu Oktoba Saba  mwaka jana.

Kulingana na UNRWA, maelfu ya familia zimelazimika kutafuta makazi katika majengo yaliyoharibiwa vibaya huko Khan Younis jiji ambalo liko kaskazini mwa Rafah, na linakadiriwa kuwa na watu wapatao milioni 1.7.

Imeripotiwa kwamba makao yote 36 ya UNRWA huko Rafah sasa yamesalia matupu.

Hayo yanajiri huku utawala haramu wa Israel ukiendeleza mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, Wapalestina zaidi ya 36,500 wameuawa shahidi na wengine 82,700 wamejeruhiwa tangu kuanza mauaji ya umati ya utawala wa Kizayun dhidi ya Wapalestina tarehe 7 Oktoba, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.